Monday, April 09, 2012

KIFO CHA KANUMBA: Siri zaanza kufichuka

KIFO CHA KANUMBA: Siri zaanza kufichuka
•  Vinywaji vilivyokutwa chumbani vyachunguzwa

na Waandishi wetu

HATIMAYE siri za kifo chenye utata cha msanii maarufu wa filamu nchini, Steven Charles Kanumba (28), kilichotokea usiku wa kuamkia juzi nyumbani kwake Sinza Vatcan jijini Dar es Salaam zimeanza kufichuka.
Kanumba aliyefariki ghafla baada ya kudaiwa kuanguka akiwa ndani kwake na mpenzi wake, Elizabeth Michael, maarufu kama Lulu (18), taarifa za kifo chake zimekuwa na mkanganyiko ambapo baadhi ya watu wanadai kuwa alinyweshwa sumu na wengine wakisema alipigwa na kitu chenye ncha kali kisogoni.
Hata hivyo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni, jana lilitoa taarifa ya uchunguzi wa awali likisema kuwa mbali na maelezo ya mdogo wa marehemu, Seth Bosco (24), pia panga, pombe aina ya ‘whisky’ ikiwa robo glasi na soda aina ya sprite vilionekana chumbani kwake.
Kamanda Kenyela alisema kuwa vinywaji hivyo vitapelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya vipimo na uchunguzi zaidi.
Alipoulizwa kama marehemu Kanumba alikuwa amekunywa pombe siku hiyo, Kamanda Kenyela alisema ni vigumu kubaini hilo ila ukweli wake utajulikana kwenye uchunguzi wa mwili wake (postmortem).
Akifafanua zaidi kuhusu chanzo cha kifo cha Kanumba, Kamanda Kenyela alisema kwa mujibu wa mdogo wake, Bosco, ambaye pia ni msanii wa kikundi cha The Great Filamu Production, siku ya tukio aliambiwa na kaka yake kuwa ajiandae ili amsindikize sehemu.
Alisema kuwa baada ya kumweleza hivyo, Kanumba aliingia chumbani kwake kujiandaa na kwamba baada ya muda kidogo alimwita mdogo wake chumbani kuwa kuna mgeni, ndipo Bosco akamwambia akiwa tayari angemuona.
Kamanda alisema kuwa muda mfupi baadaye Bosco anasema alisikia kelele ambapo kaka yake alikuwa akimtuhumu mpenzi wake Lulu.
Kenyela alisema kuwa Bosco alieleza kwamba alisikia sauti ya Kanumba akimhoji Lulu: “Kwa nini unawapigia simu mabwana zako wengine?”
Ghafla Bosco aliitwa na msichana huyo na kumuambia kuwa akamwangalie kaka yake amezidiwa.
Bosco alieleza kuwa aliingia chumbani na kumkuta Kanumba amelala sakafuni huku akitokwa na povu mdomoni akiwa haongei.
Alisema kuwa alitoka nje na kumwangalia Lulu, lakini hakumuona na hivyo kuamua kumpigia simu daktari wa Kanumba ambaye baada ya kufika aligundua kuwa amekwishafariki.
Kenyela aliongeza kuwa mwili wa marehemu Kanumba haukukutwa na jeraha lolote na kwamba umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili huku Lulu ambaye ni mkazi wa Tabata Relini akiendelea kuhojiwa kuhusiana na tukio hilo.
JK awafariji wafiwa
Rais Jakaya Kikwete, jana alifika nyumbani kwa marehemu Kanumba na kuwafariji wafiwa, akisema kuwa kifo chake ni pigo kwa taifa kutokana na juhudi zake alizokuwa amezianza za kuitangaza Tanzania nje katika tasnia ya filamu.
Rais ambaye alisaini kitabu cha maombolezo na kisha kuzungumza na ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu nyumbani hapo, alisema kuwa Kanumba alikuwa ni msanii anayependa maendeleo ya wengine ndiyo maana alijitolea kuwainua baadhi ya wasanii.
Aliwataka wasanii wenzake kuuenzi utaratibu huo ili nao waje wakumbukwe pindi watakapoondoka katika uso wa dunia.
Rais Kikwete aliwataka wafiwa wawe na subira huku wakiendelea kumuomba Mwenyezi Mungu awape nguvu ya kukabiliana na hali ngumu waliyonayo ya kuomdokewa na kipenzi chao.
Naye, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, leo saa tatu asubuhi anatarajiwa kuwasili nyumbani kwa marehemu Kunumba kuwafariji wafiwa kisha ataondoka kuelekea Dodoma kuhudhuria vikao vya Bunge vinavyoanza kesho.
CUF watuma rambirambi
Chama cha Wananchi (CUF), kimesema kuwa kimepokea taarifa ya kifo cha Kanumba kwa masikitiko makubwa na hivyo kuwataka Watanzania kuungana kwa pamoja katika kipindi hiki cha majonzi na kumuombea marehemu.
Taarifa iliyotolewa jana na Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Haki za Binadamu wa chama hicho, Abdul Kambaya, ilisema kuwa Kanumba ambaye alikuwa msanii muhimu, pengo lake halitazibika kirahisi katika jamii ya sanaa.
“Wananchi wote tunaamini kuwa jamii ya wasanii tumepoteza msanii muhimu ambaye pengo lake halitazibika kirahisi katika jamii yetu, hivyo CUF inaungana na Watanzania wote kwa kutoa pole kwa familia, ndugu na jamaa,” alisema.
Kuzikwa kesho
Taarifa iliyotolewa jana jioni na mmoja wa wana kamati ya mazishi, Hidi Mchome, ilisema kuwa Kanumba atazikwa kesho katika makaburi ya Kinondoni majira ya alasiri.
Mchome alisema uamuzi huo ni baada ya ndugu zake kuwasili akiwemo mama yake mzazi na kwamba salamu za mwisho za kuuaga mwili wa marehemu zitatolewa katika viwanja vya Leaders Club kuanzia saa nne asubuhi.
Mamia wafurika nyumbani
Katika siku ya pili ya maombolezo jana, mamia ya watu wa kada mbalimbali walifika nyumbani kwa marehemu kuwafariji ndugu na jamaa zake.
Kutokana na eneo hilo kuwa na idadi kubwa ya watu, Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni limeimarisha ulinzi wa kutosha ikiwa ni pamoja na kuifunga kwa muda barabara ya Sinza-Magomeni eneo la Vatican.

Source: Tanzania Daima.